Yupo Mungu aliyeumba mbingu na nchi na vyote vilivyomo. Matendo 4:24 “. . . Mola, wewe ndiwe Mungu, ndiwe uliyefanya mbingu na nchi na bahari na vitu vyote vilivyomo.” Ingawa yeye yupo kila mahali, makao yake makuu kwa sasa ni mbinguni. Zaburi 33:13 "Toka mbinguni Bwana huchungulia, Huwatazama wanadamu wote pia." Wanadamu wanajua kiasi kidogo sana kuhusu huyu Mungu ambaye ndiye asili yetu sote. Sababu ya kuwa tunajua kidogo inatokana na ajali iliyotokea mara tu tulipoumbwa, pale tulipoanguka dhambini.
Ajali hiyo ilileta utengo kati ya wanadamu na Mungu kiasi cha kukatisha mafunzo ya kumjua Mungu yaliyokuwa yanaendelea kwenye bustani ya Edeni. Mwanzo 3:24 “Basi akamfukuza huyo mtu, akaweka Makerubi, upande wa mashariki wa bustani ya Edeni, na upanga wa moto uliogeuka huko na huko, kuilinda njia ya mti wa uzima.” Kuanzia wakati huo mawasiliano ya ana kwa ana na Mungu yakakoma na mawasiliano ya aina nyingine yakachukua nafasi.
Kusudi la Mungu kumuumba mwanadamu ni ili awe kiumbe wa karibu anayeweza kuwasiliana naye. Mwanzo 1:26 “Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi.”
Hata baada ya dhambi kuingia, Mungu alitafuta njia ya kuwasiliana na wanadamu kupitia manabii. Manabii ni watu kutoka katika vizazi mbalimbali waliofunuliwa mambo yaliyofichika (yaliyopita na yajayo) yanayohusu wokovu wa wanadamu na namna wanavyopaswa kuhusiana naye ili kuupata wokovu huo. Waebrania 1:1 “Mungu, ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi.”
Kupitia kwa manabii hao ujumbe uliandikwa kwa uongozi wa Roho Mtakatifu na kutufikia sisi katika sura ya kitabu kinachoitwa Biblia. 2 Petro 1:21 “Maana unabii haukuletwa po pote kwa mapenzi ya mwanadamu; bali wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu.” Leo tunapata kufahamu mengi kuhusu Mungu kwa njia ya kusoma Biblia.
Biblia inaanza kwa kumtaja Mungu kudhihirisha kuwa iliandikwa ili kuwasaidia wanadamu kumfahamu Mungu. Mwanzo 1:1 “Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi.” Inazungumzia kwa muhtasari mahusiano ya Mungu na wanadamu kabla ya dhambi, katika kipindi cha dhambi, na baada ya dhambi kuangamizwa. Hii ndiyo kumbukumbu ya kuaminika ya historia ya dunia na wanadamu na ufunuo wa mapenzi ya Mungu usio na makosa. Mithali 30:5 “Kila neno la Mungu limehakikishwa; Yeye ni ngao yao wamwaminio.” Kama tungezingatia Neno la Mungu uongo usingepata nafasi. Yohana 17:17 “Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli.”
Madai ya watu wengine kuwa Neno la Mungu limepitwa na wakati hayana ukweli wowote. Isaya 40:8 “Majani yakauka, ua lanyauka; Bali neno la Mungu wetu litasimama milele.” Tunapitia wakati wa ajabu katika historia ambapo Neno la Mungu linapuuzwa na kuwekwa kando na badala yake mapokeao ya wanadamu yanapewa uzito mkubwa. Hii ni hila ya shetani ili watu wasielewe kile kilichofunuliwa kwenye Maandiko kwa ajili ya wokovu wao. Marko 7:13 “huku mkilitangua neno la Mungu kwa mapokeo yenu mliyopokeana; tena mwafanya mambo mengi yaliyo sawasawa na hayo.”
Hakuna fundisho la wokovu linalopaswa kuhitilafiana na fundisho la lililo kwenye Maandiko. Yohana 5:39 “Mwayachunguza maandiko, kwa sababu mnadhani kwamba ninyi mna uzima wa milele ndani yake; na hayo ndiyo yanayonishuhudia.” Maandiko kwa sehemu kubwa yanamfunua Yesu kama kiini cha wokovu wa wanadamu. Yale aliyofundisha na vile alivyoishi ni mambo muhimu kwa wote wenye kutaka kuokolewa.
Yesu alihitimisha kipindi chake cha kuishi hapa duniani kwa kutoa maagizo muhimu ya mwisho. Mathayo 28:19-20 “Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.” Yesu ametoa maagizo ambayo anataka watu wafundishwe. Mafundisho hayo wengine wanayafumbia macho na kutoyapa uzito unaostahili.
Mojawapo ya mafundisho hayo ni agizo la ubatizo. Marko 16:16 “Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa.” Agizo hili linafundisha kuwa ubatizo ni wa muhimu ili mtu aokolewe na ya kwamba ni lazima ufanywe na mtu mzima mwenye uwezo wa kuamini na si watoto wachanga wasioelewa lolote. Kwa nini agizo hili halifuatwi na baadhi ya wasomaji wa Biblia? Ama kwa nini linafanywa kwa namna isiyoelekezwa na Biblia?
Agizo bado linamtaka aliyeamini azamishwe ndani ya maji mengi kuashiria kifo pamoja na Kristo na si kunyunyiza maji kidogo eneo fulani la mwili (kichwani) kama ifanyavyo na baadhi ya wasomaji wa Biblia. Warumi 6:3 Hamfahamu ya kuwa sisi sote tuliobatizwa katika Kristo Yesu tulibatizwa katika mauti yake? Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima.
Ili ubatizo ulingane na kuzikwa ni kazima ufanyike kwenye maji tele. Biblia inataja maeneo yaliyotumika kwa ubatizo wakati wa Yesu na yote yalikuwa na sifa ya kuwa na maji ya kutosha kuzamisha. Yohana 3:23 “Yohana naye alikuwa akibatiza huko Ainoni, karibu na Salimu, kwa sababu huko kulikuwa na maji tele; na watu wakamwendea, wakabatizwa.” Hata Yesu ilimpasa kubatizwa akiwa mtu mzima na alienda mtoni Yordani kulikokuwa na maji tele. Mathayo 3:13 “Wakati huo Yesu akaja kutoka Galilaya mpaka Yordani kwa Yohana ili abatizwe.”
Yapo maagizo mengi yanayohusu wokovu ambayo yameachwa na wasomaji wa Biblia na kukumbatiwa mapokeo yasiyo na mamlaka kutoka kwa Mungu. Yesu anazungumziaje hali hiyo? Mathayo 5:19 “Basi mtu ye yote atakayevunja amri moja katika hizi zilizo ndogo, na kuwafundisha watu hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni; bali mtu atakayezitenda na kuzifundisha, huyo ataitwa mkubwa katika ufalme wa mbinguni.” Haijalishi una hadhi gani hapa duniani kile kitakachokufanya uwe rafiki na Yesu ni kufundisha watu kama alivyoagiza. Yohana 15:14 “Ninyi mmekuwa rafiki zangu, mkitenda niwaamuruyo.”
Biblia ni kitabu kilichoandikwa kwa uongozi wa Roho Mtakatifu na hivyo kinahitaji maombi mengi unapokisoma ili kukielewa. Yapo mafungu yaliyo rahisi kuyaelewa na mengine ni magumu. Mfano rahisi wa ujumbe ulio mgumu kuelewa ni ule ulioandikwa na mtume Paulo. 2 Petro 3:16 “. . . kama vile na ndugu yetu mpenzi Paulo alivyowaandikia kwa hekima aliyopewa; vile vile kama katika nyaraka zake zote pia, akitoa humo habari za mambo hayo; katika nyaraka hizo yamo mambo ambayo ni vigumu kuelewa nayo; na mambo hayo watu wasio na elimu, wasio imara, huyapotoa, kama vile wayapotoavyo na maandiko mengine, kwa uvunjifu wao wenyewe.”
Kinachohitajika ili kuelewa mambo magumu yaliyo kwenye Maandiko ni kuomba na kuishughulisha akili. Katika kuishughulisha akili mtu lazima ajiulize ujumbe huu uliandikiwa watu gani hapo mwanzo na nini ilikuwa sababu ya kuwaandikia. Kufahamu mazingira ya kuandikwa kwa ujumbe wenye utata kunasaidia kutatua mkwamo fulani wa uelewa.
Wakati mwingine kusoma maelezo yanayotangulia na yanayoendelea kwenye fungu lenye utata hutoa msaada wa kujua majadiliano yalihusu nini hasa. Hiyo ndiyo elimu inayokosekana hata kufikia mtu kudhania Maandiko yanajipinga yenyewe. Maandiko hayawezi kujipinga yenyewe. Wanadamu ndiyo wenye tabia ya kuyanyonga Maandiko. Maandiko yanatushauri kulitumia kwa halali Neno la Mungu. 2 Timotheo 2:15 "Jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa na Mungu, mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, ukitumia kwa halali neno la kweli."
Sababu nyingine inayosababisha ugumu wa kuyajua Maandiko ni nia ya kutotaka kuelewa. Ukitaka kufaidika na Biblia usilazimishe itafsiri kulingana na maoni yako. Biblia ni taa iongozayo walio gizani. Zaburi 119:105 “Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu.” Iruhusu ikuongoze siyo wewe uiongoze. Mtu anayehitaji maelekezo ya kule aendako hatarajiwi abishane na wanaomwelekeza (wanaoijua njia zaidi yake. Mithali 4:18 “Bali njia ya wenye haki ni kama nuru ing'aayo, Ikizidi kung'aa hata mchana mkamilifu.”
Si jambo la ajabu kuachana na dhana potofu baada ya kupata ufafanuzi sahihi wa kukusaidia kuendelea na safari. Neno la Mungu ni njia sahihi ya kukuhakikishia kuwa upo salama katika safari yako ya wokovu. 2 Petro 1:19 “Nasi tuna lile neno la unabii lililo imara zaidi, ambalo, mkiliangalia, kama taa ing'aayo mahali penye giza, mwafanya vyema, mpaka kutakapopambazuka, na nyota ya asubuhi kuzuka mioyoni mwenu.”
Watu wa Beroya ni mfano mzuri wa wasomaji wa Biblia wanaotakiwa. Wao walijiwekea utaratibu kuwa chochote Biblia itakachowafunulia watakitii hata kama ni kinyume na walivyokuwa wakiamini hapo mwanzo. Matendo 17:10-11 “Mara hao ndugu wakawapeleka Paulo na Sila usiku hata Beroya. Nao walipofika huko wakaingia katika sinagogi la Wayahudi. Watu hawa walikuwa waungwana kuliko wale wa Thesalonike, kwa kuwa walilipokea lile neno kwa uelekevu wa moyo, wakayachunguza maandiko kila siku, waone kwamba mambo hayo ndivyo yalivyo.”
Waberoya walikuwa wachunguzi wa Maandiko, hawakutaka jambo lolote la maana lililopo kwenye Maandiko liwapite. Walichunguza ili wajiridhishe kama dhana zinazotolewa na wahubiri na waalimu wao ndivyo zilivyo kwenye Maandiko. Walihofia kulishwa mawazo ya watu. Hata leo wapo watu wa namna hiyo ambao wanahitaji uthibitisho wa Maandiko katika kila kinachoaminiwa na wanadamu. Na mara wakigundua kuwa ndivyo kilivyo hufuata mara moja bila kujali gharama inayoandamana na uamuzi huo.
Wengine waliofanya kama watu wa Beroya ni wale wa Thesalonike. 1 Wathesalonike 2:13 “Kwa sababu hiyo sisi nasi twamshukuru Mungu bila kukoma, kwa kuwa, mlipopata lile neno la ujumbe la Mungu mlilolisikia kwetu, mlilipokea si kama neno la wanadamu, bali kama neno la Mungu; na ndivyo lilivyo kweli kweli; litendalo kazi pia ndani yenu ninyi mnaoamini.” Usitafute visingizio vya kukataa ujumbe kwa kumwangalia anayekupa ujumbe kama ni msomi au si msomi, ni mwanaume ama si mwanaume, ni mtu mzima au si mtu mzima na kadhalika. Mungu aweza kumtumia yeyote jambo la msingi ni kuwa ujumbe ule si wake bali ni wa Mungu. Mungu hatamhesabia hana hatia apuuziaye ujumbe wake kwa vile umetolewa na mtu asiyemkubali.
Usomaji na uelewa wa Neno la Mungu unatakiwa ueandane na kiwango cha ukuaji wa mtu. Kama mtoto anavyohitaji maziwa ili akue ndivyo mchanga wa Maandiko anavyotakiwa kuanza kujifunza. Anza kwa kusoma mambo rahisi kabla ya kuhangaika na mambo magumu yanayohitaji ukomavu. 1 Petro 2:2 “Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu.”
Hata wafundishaji wa Maandiko wanapaswa kuzingatia kuwafundisha wachanga mambo marahisi ya msingi yahusuyo wokovu kama Mtume Paulo alivyofanya. 1 Wakorintho 3:2 “Naliwanywesha maziwa sikuwalisha chakula; kwa kuwa mlikuwa hamjakiweza. Naam, hata sasa hamkiwezi.” Hata hivyo mafundisho magumu ni ya muhimu kwa ukuaji wa kiroho. Waebrania 5:12-14 “Kwa maana, iwapasapo kuwa waalimu, (maana wakati mwingi umepita), mnahitaji kufundishwa na mtu mafundisho ya kwanza ya maneno ya Mungu; nanyi mmekuwa mnahitaji maziwa wala si chakula kigumu. Kwa maana kila mtu atumiaye maziwa hajui sana neno la haki, kwa kuwa ni mtoto mchanga. Lakini chakula kigumu ni cha watu wazima, ambao akili zao, kwa kutumiwa, zimezoezwa kupambanua mema na mabaya.”
Mungu anakusudia kusimamisha utawala wake katika dunia hii na mwongozo wa utawala huo upo ndani ya Maandiko Matakatifu. Biblia nzima ni mkusanyiko wa vitabu vilivyoandikwa na wanadamu kwa maelekezo ya Roho Mtakatifu isipokuwa katika eneo moja ambapo Mungu mwenyewe aliweka mkono wake. Mungu alipotaka kuzitambulisha Amri Kumi za utawala wake hakuruhusu mwandamu aziandike. Alitumia kidole chake kuziandika. Kumbukumbu la Torati 4:13 “Akawahubiri agano lake, alilowaamuru kulitenda, yaani, zile amri kumi; akaziandika juu ya mbao mbili za mawe.” Amri hizi zimekuwa mwiba kwa shetani ambaye amekuwa akipambana kuzitokomeza. Ufunuo wa Yohana 12:17 “Joka akamkasirikia yule mwanamke, akaenda zake afanye vita juu ya wazao wake waliosalia, wazishikao amri za Mungu, na kuwa na ushuhuda wa Yesu; naye akasimama juu ya mchanga wa bahari.”
Zipo jitihada zinazofanyika chini kwa chini ili kuiondoa hasa ile amri ya nne inayoagiza wanadamu wote kuitunza Sabato. Jitihada hizo zinalenga kuiweka Jumapili siku iliyobuniwa na wanadamu kuwa Sabato bandia ya Mungu huku tawala za dunia zikishirikishwa katika mpango huo dhalimu. Mpango huo utapata nguvu kwa sababu watu wamepuuza usomaji wa Maandiko Matakatifu. Usalama wa wanadamu ni kurudi katika Maandiko. Waprotestanti walioipigania Biblia zamani wasikubali kurubuniwa na mapendekezo yasiyokubaliana na Maandiko hata kama yanatoka kwa mkubwa. Aliye mkubwa kuliko wote ni Mungu na maagizo yake yanapaswa kuheshimiwa na wote.
Biblia hii imepitia mitihani migumu hadi kutufikia sisi tunaoishi majira haya. Shetani amekuwa akitamani kuiangamiza ili wanadamu wasinufaike na kilichoandikwa ndani yake. Lakini Mungu amekuwa mwaminifu kuilinda na hivyo tutafanya vema sana kama tutaitumia kwa uaminifu ili ituletee wokovu. 2 Timotheo 3:15-17 “na ya kuwa tangu utoto umeyajua maandiko matakatifu, ambayo yaweza kukuhekimisha hata upate wokovu kwa imani iliyo katika Kristo Yesu. Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki; ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema.”